Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha ameeleza umuhimu wa michezo na kuwataka Wanajumuiya wa Chuo Kikuu Mzumbe kushiriki katika michezo mbalimbali inayoandaliwa chuo, ikiwa ni pamoja na kuimarisha afya kwa kuwa michezo husaidia kutuepushia na baadhi ya magonjwa. 
 
Prof. Mwegoha amesema hayo tarehe 28 Oktoba 2023 katika ufunguzi wa Bonanza la Michezo kwa watumishi wa Chuo Kikuu Mzumbe na ndaki zake (Dar es Salaam na Mbeya) lililofanyika katika viwanja vya michezo Kampasi Kuu Morogoro. 
 
Pia, Prof. Mwegoha ameweka bayana kwamba Menejimenti ya Chuo imeenza kufanya matengenezo ya miundombinu ya michezo ikiwa ni pamoja na kununua vifaa mbalimbali vya michezo kwa lengo la kuwawezesha watumishi kushiriki michezo vizuri.
 
  Kwa upande wake Afisa Michezo wa Chuo Kikuu Mzumbe Bw. Yohana Magongo, amesema Bonanza hilo ni sehemu ya kujenga afya na kujiandaa na mashindano ya Shirikisho la Michezo la Mashirika ya Umma na Kampuni Binafsi (SHIMUTA) yanayotarajiwa kufanyika Jjini Dodoma hivi karibuni. 
 
Mmoja wa washiriki kutoka Ndaki ya Mbeya Bw. John Mhanga ameishukuru Menejimenti ya Chuo Kikuu Mzumbe kwa kuandaa Bonanza hilo kwani amesema licha ya kuboresha afya za wafanyakazi, kujiandaa ya mshindano yajayo ya SHIMUTA, pia Bonanza hilo linasaidia kukutanisha wafanyakazi na kufahamiana na hatimaye kuleta mshikamono, upendo na amani baina ya wafanyakazi wa kampasi zote. 
 
Bonanza hilo ambalo hufanyika kila mwaka linahusisha michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, mpira wa pete, mchezo wa bao, mpira wa wavu, mpira wa kikapu, na kuhudhuriwa na wadau wa michezo wakiwemo Wanafunzi wa Chuo cha Ualimu Morogoro na timu ya Moro Star kama sehemu ya kujinoa kwa mashindano yajayo.
 
 ************************************
 
 
 
Mzumbe University,
P.O Box 1 Mzumbe,
Morogoro, Tanzania.
Tel: 255 (0) 23 2931220/1/2
Fax: 255 (0) 23 2931216
Cell: 255 (0) 754694029
Email: .
Go to top