Wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Antwerp Ubelgiji na Chuo Kikuu cha Kikristu cha Uganda ambao wapo katika programu ya kubadilishana Wanafunzi na Chuo kikuu Mzumbe wamewasilisha matokeo ya awali ya tafiti walizofanya kwenye maeneo ya maji, elimu na usalama wa chakula kwa kusimamiwa na wahadhiri wa Chuo Kikuu Mzumbe ikiwa ni sehemu ya mafunzo yao katika Shahada ya Umahiri ya Menejimenti ya ufuatiliaji na Tathmini.

Akizungumza katika semina ya uwasilishaji wa matokeo ya tafiti hizo iliyofanyika Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi
Kuu Morogoro mwishoni mwa wiki, Mratibu wa Mradi wa ‘ICP connect’ unaotekelezwa kwa ushirikiano baina ya Chuo kikuu Mzumbe na Chuo Kikuu cha Antwerp, Ubelgiji Dkt. Christina Shitima amesema kuwa uwasilishaji wa matokeo ya tafiti hizo ni matunda ya mkataba wa ushirikiano kati ya Chuo Kikuu Mzumbe na Chuo Kikuu cha Antwerp vilivyokubaliana kushirikiana na kubadilishana wanafunzi na wanataaluma, kutengeneza programu pamoja na kufanya tafiti

Dkt. Shitima amesema kuwa uwasilishaji wa matokeo hayo ya awali umelenga kuisaidia Serikali na Wadau kuchukua hatua madhubuti ikiwemo kutunga sera na kufanya maamuzi ya kuboresha huduma za kijamii zikiwemo maji, elimu na usalama wa chakula ambazo tafiti zake ndio zinatolewa mrejesho na wanafunzi hao.

Katika hatua nyingine, wadau mbalimbali walioshiriki katika Semina hiyo ya kutoa matokeo ya awali wameeleza kuwa tafiti hizo zitaisaidia Serikali kuandaa vyema malengo, mipango na bajeti kwa ajili ya kuzitatua changamoto zilizoibuliwa na watafiti hao na hatimaye kuboresha huduma za kijamii kwa wananchi

“Tafiti hizi zina tija kubwa sana ikiwa zitawasilishwa kwa Serikali na mamlaka zenye dhamana kwani zitasaidia kuweka mipango bora ya kuzikabili changamoto zilizoibuliwa katika sekta ya maji, elimu na chakula. Hata hivyo, tayari Serikali imeshaanza kuchukua hatua katika bajeti inayokuja kwa kuweka mipango ya kuboresha miundombinu ya shule ya msingi ya Mongwe ambako ilikuwa ni moja ya sampuli za utafiti kwenye sekta ya elimu”. Alisema Diwani wa Kata ya Mlali Mhe. Frank Mwananzeche.

Naye Mhandisi wa Mamlaka ya Maji Wilaya ya Mvomero Mhandisi Mlenge Luperitilo amesema tafiti kama hizo zinawasaidia wao kama watendaji wa Serikali kubaini changamoto kwenye maeneo ambayo yana shida zaidi na pengine wameshindwa kuyafikia kwa wakati huo na hivyo kuwekeza nguvu zaidi katika kutatua changamoto za maji.

Mhandisi Mlenge amekishukuru Chuo Kikuu Mzumbe kwa kuwazesha wanafunzi hao kufanya tafiti hizo na amewaomba watafiti wengi zaidi kujitokeza ili kushirikiana na Serikali kutatua changamoto mbalimbali za wananchi hasa kwenye sekta ya maji.

Kwa upande wao Wanafunzi hao wa kimataifa wamesema wamefurahi kupata fursa ya mafunzo ya kufanya tafiti nchini Tanzania kupitia Chuo Kikuu Mzumbe ambacho wamekielezea kuwa ni chuo bora sana kwa masomo kwani kina mazingira mazuri na tulivu ya kujifunzia na kwamba wanaamini matokeo ya tafiti waliyoyawasilisha yataisaidia Serikali na Wadau kuboresha huduma, na hivyo watakuwa wametoa mchango wao wa kimaendeleo.

“Tumekaa hapa Chuo Kikuu Mzumbe kwa wiki tano za mafunzo, tumekuwa na wakati mzuri sana katika mafunzo ya darasani, tumepata fursa ya kubadilishana uzoefu na wanafunzi wenzetu, tumetembelea vijiji na kuzungumza na wanajamii tumepewa ukarimu wa hali ya juu na wenyeji wetu kuanzia waratibu, walimu na wanafunzi.Tumefurahi sana kujifunza Chuo Kikuu Mzumbe”. Alisema Fiona Ward Shaw, raia wa Marekani na Mwanafunzi wa Shahada ya Umahiri katika Menejimenti ya Tathmini na Ufuatiliaji anayesoma Chuo Kikuucha Antwerp kilichopo nchini Ubelgiji.

Naye Vicent Manimani raia wa Congo DRC na Mwanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Kikristu cha Uganda amesema wamepata uzoefu wa kutosha utakaowasaidia katika taaluma yao na amewakaribisha wanafunzi wengine kutafuta fursa ya kutembelea na kujifunza katika Chuo kikuu Mzumbe kwa kuwa ni chuo kizuri sana.

“Mzumbe ni njema sana kwa kujifunzia, ninawakaribisha watu wengine kutembelea na kujifunza hapa, hakuna matata”. Alisema Vicent Manimani.

 

*****

 

 

 

 

 

 

 

Mzumbe University,
P.O Box 1 Mzumbe,
Morogoro, Tanzania.
Tel: 255 (0) 23 2931220/1/2
Fax: 255 (0) 23 2931216
Cell: 255 (0) 754694029
Email: .
Go to top